Dondoo za ufugaji bora wa
kuku wa asili
Ufugaji wa kuku wa
asili ni nyenzo muhimu katika kupambana na wimbi la umasikini kwa kuongeza
kipato cha kaya. Hata hivyo, pamoja na soko la uhakika, bado ufugaji kuku
haujaweza kutumika ipasavyo kupambana na umaskini unaowakabili Watanzania
wengi. Ni mazoea kwa jamii nyingi hapa Tanzania kufuga kuku wa asili kama
sehemu ya mila na desturi zao. Kuku wa asili amekuwa akifugwa bila ya kupatiwa
huduma muhimu kama makaazi bora, chakula cha ziada, tiba, kinga za magonjwa
mbali mbali. Muhtasari huu unatoa muongozo wa ufugaji wa kuku wa asili ili
uweze kuzalisha na hatimae kukuza kuku kwa wingi.
Dondoo ya 1
Usafi wa vyombo na
mazingira ya kuku
Uchafu ni mama wa
magonjwa, hivyo zingatia haya;
1. Vyombo vya chakula na maji visafishwe mara kwa mara kwa maji
safi na sabuni.
2. Pumba au chakula kilicholowana na kuchanganyika na kinyesi
cha kuku kitolowe na kufukiwa.
3. Choma moto au zika kwenye shimo refu kuku waliokufa kwa
ugonjwa.
4. Usifuge kuku na ndege wa jamii nyingine kwa mfano bata
katika banda moja.
5. Ondoa mbolea mara kwa mara kutoka katika banda la kuku.
6. Tumia dawa za kuulia vimelea kusafishia banda na upake
chokaa angalau mara moja kwa mwaka.
7. Ziba matundu yote yanayoweza kuruhusu panya na wanyama
wakali kama vicheche kuingia katika banda la kuku.
Dondoo ya 2
Magonjwa na kinga kwa kuku
wote
Ndui ya kuku
Huathiri sana
vifaranga wanaokua na ujitokeza kwa wingi wakati wa mvua za muda mrefu.
Husababisha vivimbe katika uso/ kishungi na hata sehemu nyengine zisizo na
manyoya.
Mdondo/kideri
Mdondo, au kwa majina
mengine lufuo, au kideri ni ugonjwa hatari katika magonjwa ya kuku wa asili. Ni
ugojwa wa virusi ambao huathiri kuku wa rika zote, huweza kuangamiza kuku wote
kijijni.
Ukosefu wa vitamini A
Ugonjwa huu
husababisha macho kuvimba na kutoa uchafu mziito kama sabuni iliyolowana. Kuku
wenye dalili hizi hawaponi na hata kufa. Ugonjwa hujitokeza baada ya kipindi
kirefu cha kiangazi kwa ajili ya ukosefu wa majani mabichi.
Kosidiosisi
Huathiri kuku wa umri
wowote lakini huuwa zaidi vifaranga na kuku wanaokua. Kuku hudhoofika, manyoya
huvurugika na kuku huwa kama wamevaa koti. Kuku huarisha damu au kinyesi cha
kahawia na huzubaa na kuonekana kama wamevaa koti.
Viroboto, chawa na utitiri
Hawa ni wadudu wa nje
wanaoshambulia ngozi. Huweza kusababisha ugonjwa kutokana na kunyonya damu.
Viroboto hushambulia kichwa na kunata huku wakinyonya damu. Viroboto huuwa
vifaranga. Chawa na utitiri hughasi kuku hadi wakashindwa kutaga na kuatamia.
Minyoo
Minyoo huweza
kudhofisha kuku na kuwafanya waweze kuugua maradhi mengine kirahisi. Muone
mtaalaam ukihisi kuku wako wana minyoo.
Dondoo ya 3
Chakula cha ziada
1. Wapatie vifaranga nyongeza ya protini kwa kuwachanganyia
vumbi la dagaa au vichwa vya dagaa vilivyotwangwa kwenye pumba za mahindi.
2. Changanya kikombe kimoja cha vumbi la dagaa na vikombe
vitano vya pumba za mahindi (tumia kikombe kidogo cha chai).
3. Mchwa na wadudu wengine wanaweza kutumika kama nyongeza ya
protini.
4. Vuna mchwa kwenye vichuguu au tengeneza mchwa katika njia za
mchwa.
5. Kutengeneza mchwa: changanya kinyesi cha ng’ombe na majani
makavu, mabua ya mahindi au maranda ya mbao katika chungu au ndoo ya zamani.
6. Mwagia maji hadi kila kilichomo kilowane kisha weka katika
chombo kama ndoo au chungu. Weka chombo chako katika njia ya mchwa ukikigeuza
juu chini na subiri hadi kesho yake asubuhi, kisha beba vyote vilivyomo na
uwamwagie kuku mahali walipo.
Dondoo ya 4
Utotoleshaji wa vifaranga
Chagua jogoo bora na
tetea bora kuzalisha kuku.
Sifa za jogoo bora
1. Awe na umbo kubwa, awe ukiko mzuri na usioangukia upande
mmoja.
2. Apende kuwa na himaya yake. Ukimpata jogoo mwenye sifa hizi
mueke yeye na matetea kumi. Hivyo ukiwa na matetea ishirini jogoo wawili
wanatosha.
Sifa za tetea bora
Tetea bora ni yule
mwenye umbo kubwa, mwenye uwezo wa kutaga mayai ya kutosha, kuatamia na
hatimaye kutotoa vifaranga.
Uhifadhi wa mayai
1. Weka mayai mahali safi na penye hewa ya kutosha.
2. Tumia kasha lililokatwa na kujaza mchanga mkavu na safi au
kasha la kuhifadhia mayai.
3. Weka sehemu butu ya yai iwe upande wa juu na ile
iliyochongoka itizame chini.
4. Andika namba au tarehe katika siku lilipotagwa.
5. Mayai yakishatagwa yatolewe na kuhifadhiwa na moja liachwe
kwenye kiota ili kumuita kuku kuja kutaga kesho yake.
Kuatamiza mayai
1. Kuku awekewe mayai yatakayokuwa na uwezo wa kuyaatamia na
kuyatotoa yote.
2. Mayi 10 hadi 12 yanatosha kuatamia.
3. Mayai ya kuatamiza yasizidi wilki 2 toka kutagwa.
4. Yai la mwisho kutagwa liwe la kwanza kuchaguliwa hadi
yapatikane mayai 10 mpaka 12, na apewe kuku wa kuyaatamia.
5. Mayai ya kuatamiza yasafishwe kwa kitambaa kikavu na safi au
kilichowekwa spiriti
Kutotolesha vifaranga wengi
kwa wakati mmoja
1. Kama unataka kuku zaidi ya mmoja watamie na kutotoa kwa
mpigo fanya yafuatayo;
2. Kuku wa kwanza akianza kuatamia muwekee mayai yasiyo na
mbegu mfano mayai ya kuku wa kisasa au kuku asiye na jogoo.
3. Rudia zoezi hilo hadi utakapofikisha kuku watano kisha
wawekee kuku wote mayai yenye mbegu.
Dondoo ya 5
Matunzo ya vifaranga ili
kuzuia vifo
Vifaranga wengi hufa
kabla ya kufikisha miezi miwili kutokana na magonjwa, baridi na kuliwa na
wanyama wengine. Ili kupunguza vifo vya vifaranga wa siku 1 hadi miezi miwili
zingatia yafuatayo;
Ulinzi dhidi ya mwewe na
wanyama wengine
1. Weka vifarang kwenye tega na kuwafunika ili wasinde mbali
wakati wa mchana. Wape maji na chakula. Hakikisha hawapigwi jua wala kunyeshewa
mvua. Wakati wa usiku walale na mama yao.
Chanjo ya mdondo
kideri/lufuo
Kama tetea alichanjwa
kabla ya kuanza kutaga vifaranga wanaoanguliwa huwa na kinga ya mdondo ya
kuwatosha kwa wiki 3 za kwanza za maisha yao. Wachanje vifaranga hao dhidi ya
mdondo wafikishapo umri wa siku 18.
Vifaranga ambao
historia ya chanjo ya mama haijulikani, wapewe chanjo ya mdondo siku tatu baada
ya kuanguliwa, rudia hadi wakifikisha wiki tatu kisha uchanje kila baada ya
miezi 3
Kinga dhidi ya kosidiosisi
Kinga ya kosidiosisi
kwa vifaranga, itolewe hata kama ugonjwa haujajitokeza.
1. Wape dawa ya amprolium kwa muda wa siku tatu mfululizo mara
wafikishapo siku saba tokea waanguliwe kama kinga ya kosidiosisi.
2. Dawa inaweza kutolewa hata kama wamevuka umri huo. Fuata
maelekezo ya mtaalam juu ya kiasi cha dawa kinachopaswa kuchanganwa katika maji
au pumba
3. Kama vifaranga wadogo wataonesha dalili za kuzubaa kama
kuvaa koti wapewe dawa ya amprolium kwenye maji kwa utaratibu ufuatao;
Dawa siku tatu
mfululizo: usiwape kwa siku mbili; gawa tena kwa siku tatu
Hitimisho
1. Hakikisha banda na vyombo vya chakula cha kuku ni visafi
kuepusha magonjwa.
2. Usichanganye kuku na bata katika banda moja
3. Lisha chakula cha ziada hasa kwa vifaranga.
4. Kideri, kosidiosisi, ndui na upungufu wa vitamini A ni
vyanzo vikuu vya vifo vya kuku wako. Kumbuka kukinga kuku wako dhidi ya magojwa
haya.
5. Kumbuka kuchagua mayai ya kuatamiza kama ilivyoelekezwa ili
kuepuka kupata mayai viza.
6. Vifaranga wadogo hadi wiki nane huhitaji matunzo mazuri,
fuata maelezo kuzuia vifo.
7. Kumbuka ukiuza kuku wengi kwa mpigo utaongeza mapato yako,
jitahidi kuzalisha vifaranga kwa wingi ili upate kuku wengi baadae.
8. Muone mtaalam wa mifugo ulie karibu nae kwa ushauri zaidi.
9. Soma maelezo haya mara kwa mara na ufanye yalioelekezwa.
10.
Washirikishe wengine
katika kaya yako ili nao wajifunze na kufanya hivyo kukuza ufugaji na kipato
cha familia.
Chanzo ufugajimakini.blogspot.com
Comments
Post a Comment