Skip to main content

KILIMO CHA KISASA CHA MPUNGA

Utangulizi


Mpunga ni zao la pili la chakula kwa umuhimu linalolimwa sehemu nyingi nchini Tanzania. Umuhimu wa zao hili umeongezeka kuanzia muongo uliopita kutokana na jamii za mijini na vijijini kupendelea zaidi kula wali na kupunguza ulaji wa vyakula vingine na kulifanya zao hili kuwa la chakula na biashara.

Mvua ni chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga. Viwango vya mahitaji ya maji katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za mpunga. Ni kwa jinsi hii mpunga hupandwa katika mazingira mbalimbali kutegemea na mahitaji yake ya maji. Zipo aina tatu kuu za mazingira yanayolimwa mpunga kulingana na upatikanaji wa maji na hali ya mwinuko wa nchi. Mazingira haya ni kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea mvua (72%), kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko (20%) na kilimo cha mpunga cha umwagiliaji (8%).

Kiasi cha mpunga kinachozalishwa nchini kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka tani 41,000 mwaka 1970 hadi tani 811,500 mwaka 1998. Ongezeko hili limetokana na kuongezeka kwa eneo linalolimwa mpunga na kwa kiasi kutokana na kuongezeka kwa miradi midogo ya umwagiliaji pamoja na matumizi ya tekinolojia bora za kilimo.

Maeneo yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania: ni Morogoro maeneo ya bonde la kilombero/Ifakara, Dakawa, Malolo; Mbeya: Kyela, Mbarali; Shinyanga: Kahama; Mwanza, Bonde la Ruvu mkoani Pwani. Na maeneo mengine mengi

shamba-la-mpunga
Shamba la mpunga

pH ya udongo (Soil pH)

pH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa tindikali (ph ndogo kuliko 7), nyongo (ph kubwa kuliko 7), au katikati (neutral) - ph ya 7. Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0). Mpunga hustawi kwenye udongo wa mfinyanzi wenye tindikali ya wastani na virutubisho vya kutosha.
Kuandaa Shamba, Kupanda na Kupalilia

Kuandaa shamba, kusafisha, kulima/kutifua

Ni vyema mashamba yaandaliwe mapema kabla ya msimu wa kupanda haujaanza ili kumpa mkulima fursa ya kupanda kwa wakati unaotakiwa. Kuna njia mbalimbali zinazotumika kuandaa mashamba. Kati ya njia hizi ni pamoja na kufyeka, kung’oa visiki na kulima. Shamba linaweza kulimwa kwa kutumia:
  • Jembe la mkono - wengi wanatumia
  • Jembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombe
  • Power tillers
  • Matrekta

Baaada ya kulima, shamba linawekwa maji ili liloane vizuri na kisha udongo unachanganywa vizuri na maji ili kutengeneza tope. Hii ni kuchavanga (puddling). Hii inarahisisha:
  • Kupandikiza miche
  • Kuhifadhi maji

Mbegu Bora za Mpunga

Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:

Mbegu za asili za mpunga: Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimo. Kuna aina nyingi za mipunga ya asili inayolimwa sehemu mbalimbali hapa nchini kama Supa, Kahogo, Kula na Bwana, Shingo ya mwali, n.k. Wakulima wanazipenda mbegu hizi kutokana na kuwa na sifa kama vile ladha nzuri, uvumilivu wa matatizo mbalimbali ya kimazingira na kwa sababu ya uwezo wa mbegu hizi kustahimili katika hali mbaya ya hewa na hazihitaji uangalizi wa hali ya juu.

Sifa hizi ni matokeo ya mbegu hizi kumudu mazingira na uchaguzi wa mbegu uliofanywa na wakulima kwa miaka mingi. Hata hivyo, nyingi ya mbegu hizi zina uwezo mdogo wa kuzaa, zinachelewa kukomaa, ni ndefu na rahisi kuanguka.

Mbegu zilizoboreshwa: Hizi ni zile zilizoboreshwa kutokana na mbegu za asili. Mfano wa mbegu zilizoboreshwa ni kama vile Katrin, IR54, na IR64. Zinazaa sana hasa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo, hazikidhi ladha ya walaji na ukobolekaji wake si mzuri na baadhi hazistahimili kwenye mazingira mengi ya kawaida. Hii imezifanya mbegu hizi kukubalika na wakulima kwa kiwango kidogo sana.

Mbegu bora nyingine zilizozalishwa kutoka utafiti na kuonekana kupendwa kwa ajili ya mavuno mengi na ladha nzuri kama TXD88 na TXD85. Hivi karibuni imetolewa mbegu nyingine iitwayo TXD306 (SARO5), mbegu hii hupendwa na wakulima, wafanyabiashara na walaji kutokana na sifa yake ya mavuno mengi, punje ndefu kiasi na nzito, ladha nzuri na yenye kunukia pindi ipikwapo na kuliwa.

Mbolea za kupandia mpunga

Kabla ya kuweka mbolea hakakisha kuwa majaruba yanatengenezwa ili kuhakikisha maji hayaingii na kutoka kiholela. Mbolea ya kupandia huwekwa kwa kusia katika jaruba kabla ya kuchavanga. Kuchavanga husaidia kuchanganya udongo na mbolea na pia kutengeneza eneo zuri la kupandikiza miche. Baadaye miche hupandikizwa.

Viwango vya mbolea za kupandia mpunga
Kiwango cha mbolea za kupandia kilichopendekezwa ni kilo 20 phosphate (P) kwa hektari ambayo ni sawasawa na kiasi mifuko mitatu kwa hekta ya DAP (= mfuko mmoja kwa ekari), au mifuko miwili kwa hekta ya Minjingu Phosphate (= mfuko mmoja na nusu kwa ekari) au mifuko minne na nusu kwa hekta ya Minjingu Mazao (= mifuko miwili kwa ekari).

Jinsi ya kupanda mpunga Kitaalam

Kuna njia mbili kuu zinazotumika kupanda mpunga shambani. Njia hizo ni ile ya kupanda mbegu moja kwa moja shambani na ile ya kupandikiza miche.

  • Kupanda mbegu moja kwa moja
Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu moja kwa moja kwenye shamba lililotayarishwa vizuri. Njia ya kawaida waitumiayo wakulima ni ile ya kumwaga na kufukia mbegu (broadcasting). Njia zingine ni zile za kupanda mbegu kwenye mashimo yaliyo kwenye mstari na kwa kuzingatia nafasi maalum au mbegu hupandwa kwenye mashimo bila kufuata mstari na bila kuzingatia nafasi iliyopendekezwa (dibbling). Vile vile mbegu hupandwa kwa kunyunyizwa kwenye vifereji vyenye vina vifupi na kufukiwa pasipo kuwa na nafasi kati maalum kati ya punje na punje (seed drilling)

  • Kupandikiza miche
Njia hii hutumika kwa kupanda mbegu kwanza kwenye kitalu kabla ya kuzihamishia shambani. Mara nyingi mbegu zetu hutumia wiki tatu hadi nne baada ya kuota kwenye kitalu na kufikia umri wa kupandikizwa shambani. Katika shamba la mpunga miche hupandikizwa shambani kwenye mstari na kwa nafasi maalum au kupandikizwa holela bila kuzingatia nafasi maalum za kupanda.

Inashauriwa kupandikiza miche katika kina cha sentimeta 2 hadi 3. Ukipanda kina kirefu machipukizi huchelewa kujitokeza. Baada ya kupandikiza miche, machipukizi hujitokeza baada ya siku 5 hadi 10.

Kupandikiza-miche-ya-mpunga
Kupandikiza miche ya mpunga


Nafasi ya kupanda mpunga

Nafasi ya kupanda mpunga mbegu bora ni sm 15 kwa sm 15 au sm 20 kwa sm 20. Kwenye mpangilio wa mistari miwili miwili (double rows), nafasi kati ya mistari miwili ni sm 10, nafasi kati ya mmea na mmea katika kila mstari ni sm 20, na nafasi kati ya mistari miwili na mistari miwili mingine (double rows) ni sm 40. Mbegu za asili zipandwe kwa nafasi ya sm 20 kwa sm 20 au sm 25 kwa sm 25 au sm 30 kwa sm 30.

Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo.

Muda wa kupanda

Muda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia desemba hadi januari kwa mpunga wa muda mrefu. Kwa mpunga wa muda wa kati na muda mfupi, tarehe ya kupanda ni februari hadi machi.

Kupalilia Mpunga

Ni muhimu shamba lipaliliwe ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno.

Katika kilimo cha mpunga, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Ni vizuri katika kilimo cha mpunga, shamba lipaliliwe mara mbili, kutegemeana na hali ya magugu katika shamba. Unaweza kupalilia kwa kung’olea kwa mkono, kwa mashine au kwa kutumua viua magugu (herbicides) kama vile 2, 4-D (Two Four D).

Utafiti unaonyesha kwamba, shamba la mpunga ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.

Mbolea za kukuzia mpunga

Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni.

Kiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ya UREA au Minne na Nusu Ya CAN au Mitatu ya SA. Mbolea inayotumika mara kwa mara ni Urea. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium. Kwenye mpunga, mbolea ya kukuzia inawekwa wiki mbili baada ya kupandikiza miche na irudie tena baada ya wiki nne.
 
Kuweka mbolea: Mbolea ya kukuzia hutiwa kwa kusia wiki mbili baada ya kupandikiza, na kurudia mwezi mmoja baadaye. Ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili ya kiasi kinachopendekezwa.

Mpunga-uliopandwa-kwenye-mistari
Shamba la mpunga uliopandwa kwa mistari

Kudhibiti Magonjwa na Wadudu Wanaoshambulia Mpunga

Magonjwa Yanayoshambulia Mpunga

Magonjwa ya mpunga yamegawanyika katika makundi matatu kulingana na vimelea visababishi ambavyo ni fungasi, virusi na bakteria.
i) Rice blast (Ukungu)
Unaosababishwa na Pyricularia oryzae.
Dawa/Kudhibiti: Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe (white flies).

ii) Brown leaf spot
Unaosababishwa na Helminthosporium spp.
Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu kwa udongo unaofaa, weka mbolea ya kuzuia au tibu mbegu na dawa.

iii) Sheath rot
Unaosababishwa na Acrocylindrium oryzae.
Dawa/Kudhibiti: Kwa sasa hakuna njia ya kuzuia

iv) Rice Yellow Mottle Virus (RYMV) - Kimnyanga
Hivi karibuni ugonjwa wa kimyanga umetajwa kama ugonjwa hatari sana kwa mpunga hapa Tanzania.
Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu zilizoboreshwa, zinazostahimili magonjwa au ng’oa mimea iliyoathirika.

Magonjwa yasababishwayo na bakteria nayo wametajwa kuwa na madhara makubwa kwa uzalishaji wa mpunga hapa nchini. Bakteria hawa wanajumuisha Acidovorax avenae subsp. Avenae asababishae ugonjwa wa bacterial stripe, Pantoea aglomerans, asababishae ugonjwa wa palea browning na Xanthomonas oryzae p.v. oryzae.

 

Wadudu wanaoshambulia mpunga

Kuna aina nyingi sana za wadudu wanaoathiri mpunga katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mpunga. Wanapokithiri na wasipodhibitiwa hupunguza kiasi cha mavuno shambani.

i) White flies (Funza weupe)
Dawa/Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Regent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid)

ii) Rice stalk borer waharibifu
Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Re­gent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid) Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea na njia zinginezo.

Kuvuna, Kukausha, Kusafisha na Kuhifadhi

Kuvuna: Mpunga uko tayari kuvuna wakati asilimia themanini (80%) ya rangi ya mpunga kwenye masuke imebadilika na kuwa dhahabu. Mpunga unavunwa kwa kukata bua pamoja na suke lake.

Uvunaji-wa-mpunga
Uvunaji wa mpunga

Kukausha: Rundika pahali pakavu k.m. kwenye tuta la jaruba halafu pigapiga (thresh) ili kutenganisha masuke na mpunga. Kama mpunga hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi juani kwa siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mpunga ukauke vizuri ili usioze ukiwekwa ghalani.

Kusafisha: Mpunga uliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mapepe huondolewa. 

Kuhifadhi: Mpunga safi huwekwa kwenye gunia na magunia kupangwa vizuri ghalani juu ya mbao yasiguse sakafu.
                                       CHANZO :mogriculture.blogspot.com

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

Njia 3 za kuagana na maumivu ya jino haraka

Kwa kawaida hushauriwa kuwaona wataalam wa meno pale unapopata maumivu makali ya meno, lakini zipo njia za asili kadhaa ambazo huweza kupunguza ukali wa maumivu ya meno. Kama wengi wetu tunavyofahamu mara nyingi maumivu ya meno hutokea zaidi nyakati za usiku ambapo unakuwa huwezi kabisa kufika hospitali kwa ajili ya kuwaona wataalam wa meno au kung'oa kabisa na ndio maana leo nimeona nikufundishe mbinu hizi ya kupunguza maumivu hayo wakati ukisubiri kukuche ili ufike hospitali. 1. Kwanza kabisa unaweza kutumia kitunguu swaumu Hiki ni kiungo ambacho huweza kufananishwa na antibiotic kutokana na uwezo wake wa kuua vijidudu haraka. Unachopaswa kufanya ni kusaga kitunguu swaumu chako kisha changanya na chumvi kiasi halafu tumia mchanganyiko huo kwa kuweka moja kwa moja kwenye jino lenye maumivu au tatizo. 2. Pia unaweza kutumia kitunguu maji Hiki utakitafuna taratibu hususani  kwenye eneo lenye jino ambalo linasababisha maumivu kwa wakati huo, lakini pia kama kuta

Faida 27 Za Kiafya Zipatikanazo Kwa Kutumia Asali Na Mdalasini

MDALASINI NA ASALI Asali inafahamika vema Duniani kote kama mojawapo ya silaha ya kiajabu katika kupigana na magonjwa na matatizo yatokanayo na uzee. Sasa hivi, utafiti mpya umeonyesha kwamba uwezo wa asali unaweza kuongezwa maradufu kama itachanganywa na mdalasini wa kawaida. Uchunguzi wa kina ufanywao kwa wiki na jarida la World News wa Tiba, wataalamu wa madawa yatokanayo na mimea pamoja na kijarida cha afya na lishe, imeonekana kwamba kuna dazani nyingi za umuhimu wa asali na mdalasini pamoja na michanganyiko {dawa} ya kusisimua iletayo afya bora. Kama ifuatayo: 1. Ugonjwa wa Viungo/Maumivu na Uvimbe {ARTHRITIS}. Wataalamu wa lishe wanapendekeza kuchukua kwa kutumia mchanganyiko wa sehemu moja ya asali pamoja na sehemu mbli za maji vuguvugu na kijiko kimoja {cha chai} chenye mdalasini - na kuchua sehemu zilizoathirika. Nafuu hupatikana katika muda wa dakika moja. Vinginevyo tengeneza chai-kikombe kimoja chenye maji moto, weka vijiko vya chakula -viwili vya as

Vyakula 4 vya kuongeza hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake

Wanawake wengi wanaokaribia ukomo wa hedhi au waliokoma hedhi tayari(menopause) hukosa hamu ya tendo la ndoa. Wataalamu wa afya wameshauri vyakula vinavyoweza kuwapa wanawake hamu  ya tendo la ndoa. Mtaalamu wa Saikolojia wa Uingereza, Cassie Bjork, anasema badala ya kutumia dawa (Viagra) vya kuongeza hamu ya tendo la ndoa kuna vyakula maalum. Spinachi Wataalamu hao wanasema mboga ya majani aina ya spinachi ina wingi wa madini ya magnesium ambayo husaidia kusambaza damu kwenye mirija. Damu inaposambaa vyema mwilini hata hamu ya tendo la ndoa huongezeka. Bjork anasema kula kwa wingi mboga hizo kunamsaidia mwanamke hata kufikia kilele. Chai ya Kijani (Green tea) Chai ya kijani ina kompaundi iitwayo catechins. Hii inaelezwa kuwa inasaidia kuyeyusha mafuta mwilini. Lakini pia inalisaidia ini  kuchuja sumu na kuisaidia mishipa ya damu kufanya kazi vizuri. Damu ikitembea vyema mwilini, ni rahisi kwa mwanamke kujisikia hamu ya tendo.  Mafuta ya samaki  Zipo aina nyin