Kama wewe ni mjasiriamali au unapenda ujasiriamali basi moja kati ya malengo yako ni kufikia utajiri. Hamu hii ya kufikia utajiri inatufanya tupige kazi usiku na mchana bila kuchoka. Tunapowaona wale waliotajirika tayari tunatamani kujua siri zao za mafanikio ili na sisi tuweze kuwa kama wao au zaidi. Mimi binafsi nimekuwa na hamu kubwa ya kujua siri hizi toka nina miaka 12. Ni muda huo ambapo nilianza kusoma vitabu mbalimbali vya wafanyabiashara na kufuatilia maisha yao kiujumla. Toka muda huo na hadi sasa nikiwa nimetimiza miaka 21 nimegundua kuwa kuna vitu vitano vikuu ambavyo wajasiriamali matajiri huwa navyo ambavyo vimewawezesha kufikia hapo walipo.
1. USHAWISHI
Ujasiriamali sio spotispoti. Masaa mengi ya kazi, hatari ya kutofanikiwa na misukosuko ni kawaida. Kuamua kujikita katika jambo hili ni kati ya maamuzi magumu mtu unaweza kufanya. Hii ni kwa sababu kama una familia basi muda na familia yako utapungua sana. Kama wewe ni mtu wa marafiki na viwanja basi itabidi upunguze. Na zaidi ya hapo mara nyingine wakati unaanza biashara au wakati tayari umeshaanza utahitaji kushawishi watu wakufanyie mambo mbalimbali. Umshawishi mtu anunue bidhaa yako, umshawishi ofisa wa benki akupe mkopo au umshawishi rafiki yako aungane nawe katika biashara yako. Ni ushawishi kila sehemu. Bila ushawishi huwezi kusogea mbele katika ujasiriamali.
2. JINSI YA KUAJIRI WATU WANAOFAA
Ni rahisi sana biashara kusambaratika kwa sababu ya wafanyakazi wabovu. Juzi kati moja ya watu ninaowafahamu ilibidi amfukuze msimamizi wake wa saluni kwa sababu hakuwa mwaminifu katika mauzo ya saluni. Kuna uwezekano mkubwa wewe pia ukawa umesikia stori kama hizi mtaani. Hebu sasa fikiria kama mtu kama Mengi angekuwa na watu kama hawa katika kampuni yake ingewezekana kufika hapo alipo leo? Jinsi ya kutambua mfanyakazi bora ni kati ya sehemu muhimu sana katika kukuza biashara. Wafanyakazi wazuri watakuza mauzo yako. Wafanyakazi wazuri watakufanya uwe tajiri. Lenga kujenga uwezo huu na utafika mbali sana katika safari hii ya ujasiriamali.
3. JINSI YA KUTUMIA MUDA WAO VIZURI
Katika siku moja kuna masaa 24. Hakuna siku utaongezewa hata sekunde moja. Na yakipita hayarudi tena. Kama mjasiriamali huwa najiuliza swali moja ninapoamka. Leo nitafanya nini kuboresha biashara yangu? Vitu vingine ambavyo najiuliza mara kwa mara ni nimepoteza muda wapi leo? Nifanye nini ili kitu hiki kichukue muda mfupi zaidi kumaliza? Nimpe nani kazi hii ili muda huu niutumie kufanya kitu muhimu zaidi? Ni maswali haya ambayo yananipelekea kuepuka kuingia Youtube kwa sababu huwa naishia kutumia muda mwingi humo halafu sifanyi cha maana. Ni maswali haya ambayo yananipelekea kutafuta mbinu za kufanya vitu haraka zaidi kila siku. Ni maswali haya ambayo yananipelekea nilipe watu wafanye kazi mbalimbali ili niwe huru kufanya mambo ya muhimu kama kuandika makala hii. Hebu kaa ufikirie je leo umetumia muda wako vizuri? Kumbuka, kushinda instagram ukifuatilia vita ya yule dada wa Marekani na serikali hakutazogeza biashara yako mbele. Kama hutaki kabisa kupitwa na ubuyu tenga dakika tano kwa siku kuchungulia inatosha…
4. MATUMIZI MAZURI YA PESA
Ukichunguza matajiri wajasiriamali utaona kuwa wanaheshimu utajiri wao. Wanajua kuwa kupata pesa tu haitoshi inabidi uweze kuitunza pesa vizuri na kisha uitumie hiyo pesa uliyoitunza kupata pesa nyingi zaidi. Utaona watu hawa ambao wengi wameanza wakiwa na mitaji midogo au bila kitu kabisa wakikuza mitaji yao taratibu na hadi wanafikia utajiri mkubwa hawana matumizi ya ovyo ya pesa. Mengi, Bakhresa, Dewji, Rostam Aziz ni kati ya wajasiriamali wakubwa nchini. Kwa pesa walizonazo wanaweza kubadilisha magari ya kifahari kila wiki kwa mwaka mzima. Wanaweza kumiliki nyumba za kifahari katika kila mkoa. Wanaweza kununua Iphone 7 za kutosha wakawa wanabadilisha kila siku. Ila hakuna anayefanya hivyo. Japokuwa tayari ni matajiri bado sehemu kubwa ya kipato chao kinaenda katika kukuza biashara zao. Wanaheshimu pesa. Kama mjasiriamali tambua kuwa biashara yako ndio maisha yako. Tumbua pesa zako na biashara yako itakufa. Rudisha kipato katika biashara na utatajirika kupita mategemeo yako
5. KUWA NA FUJO TULIVU
Wote tunamjua angalau mtu mmoja ambaye ana fujo sana. Huyu ni yule rafiki yako ambaye ugomvi ukitokea aidha kauanzisha au yupo mstari wa mbele kwenye mapigano. Huyu ni yule mbishi ambaye hakubali kushindwa. Yakitokea mabishano tu basi ukiwa upande wake ushashinda. Katika ujasiriamali unahitaji kuwa na fujo. Ila hapa nimeongelea fujo tulivu. Namaanisha nini? Utakutana na misukosuko katika biashara. Mtu mwenye fujo tulivu atapigika, kisha atanyanyuka na kuendelea kusonga mbele bila kulalamika. Safari kuelekea utajiri itachukua muda mrefu kuliko unavyodhania. Mtu mwenye fujo tulivu hatakata tamaa na kuishia njiani, ataendelea kupiga kazi mpaka kieleweke. Kuna kipindi washindani watataka kukuchukulia wateja wako. Mtu mwenye fujo tulivu hataenda kuanzisha timbwili katika ofisi za washindani wake, bali atapigana kuboresha huduma zake ili abakize wateja wake na aongeze wengi zaidi. Kichwani mwa mtu mwenye fujo tulivu tayari yeye ashakuwa tajiri. Hajali changamoto, hajali misukosuko, hajali chochote. Yeye kashaweka lengo la kufikia utajiri na hakuna kitu duniani au kwingineko kitamzuia kufikia lengo lake. Kichwani mwake hadi Mungu tayari yupo katika upande wake hivyo hawezi kushindwa.
Hivyo ndivyo vitu vitano vikuu ambavyo matajiri wajasiriamali wanavyo. Kama wewe pia unataka kuwa tajiri basi hii ni fursa kwako ya kuanza kujifunza vitu hivi vikuu ili uweze kusogea karibu zaidi na lengo lako ya kuwa tajiri.
Comments
Post a Comment