MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya mabadiliko katika mfumo wa
usimamizi wa matumizi ya Mashine za kielektroniki za Utoaji risiti
(EFDMS) ili kudhibiti uwezekano wa kughushi risiti.
Aidha, mfumo huo una usalama wa hali ya juu, kwani miamala na risiti
zote zitakuwa na saini ya kielektroniki na “QR Code”, hivyo kupunguza
uwezekano wa kughushi risiti kutoka kwenye mashine za kielektroniki
ambazo hazijasajiliwa na mfumo wa mamlaka hiyo.
Akizungumza wakati wa kufungua semina ya Walipakodi Wakubwa, Kaimu
Kamishna Mkuu wa TRA, Neema Mrema alisema mfumo huo ni wa kiintelijensia
kwani una uwezo wa kutambua hati ya mauzo kwa mkopo, marejesho ya
mauzo, risiti halali na durufu.
“Mfumo umezingatia kupunguza gharama, kwani mfumo huu ni wa Tehama ambao
utaipunguzia gharama serikali kununua mashine halisi kwa kuwa
umeunganishwa na seva ya TRA,” alisema Neema.
Alisema mfumo huo pia una ufanisi mkubwa na ni rafiki kwani unaweza
kuunganishwa na mifumo mingine kama mifumo ya ankara, mauzo na
stakabadhi mbalimbali kwa kufanya mabadiliko machache, pia unaruhusu
matumizi ya fedha mbalimbali.
Semina hiyo ya siku moja imewakutanisha walipakodi wakubwa kwa ajili ya
kupata elimu juu ya Sheria ya fedha ya mwaka 2016 na Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT) ya mwaka 2014.
Mada zingine zilizowasilishwa ni kodi ya zuio katika bidhaa na huduma,
mfumo wa ukusanyaji wa maduhuli kwa kutumia mashine za kielektroniki za
utoaji risiti (vitual EFD).
Akizungumzia kodi ya zuio, Neema alisema utekelezaji wa Kodi ya zuio
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013 umekuwa na changamoto mbalimbali kwa
idara na taasisi za serikali.
Tembelea muungwana.co.tz
Tembelea muungwana.co.tz
Comments
Post a Comment