NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC,
Himid Mao ‘Ninja’, anaendelea na majaribio yake kwenye kikosi cha
Randers inayoshiriki Ligi Kuu nchini Denmark.
Himid tayari ameshafanya mazoezi mara mbili juzi na jana akiwa na kikosi
cha wachezaji wa akiba wa timu hiyo, ambapo leo Jumatano alipewa
mapumziko kabla ya kesho Ijumaa kuanza rasmi kujifua na kikosi cha
kwanza cha Randers.
Kwa mujibu wa mtandao wa klabu hiyo, umeeleza kuwa kiungo huyo nyota
mkabaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, 24, yuko tayari kwa
mara ya kwanza kucheza soka la kulipwa na kulipa kisogo soka la nyumbani
kwa kuhakikisha anapata mkataba wa kusajiliwa na Randers.
Nyota huyo ambaye atafanya majaribio ndani ya timu hiyo kwa siku 10,
aliondoka nchini Jumatatu iliyopita baada ya pande zote mbili za timu
hizo kufanya makubaliano kuhusu mchezaji huyo, ambapo mara baada ya
kumaliza zoezi hilo atarejea mara moja Azam FC kabla ya taratibu
nyingine kufuata kama watakuwa wamevutiwa na huduma yake.
Habari njema ni kuwa mbali na kufanya mazoezi na Randers, pia anatarajia
kucheza mchezo mmoja akiwa na kikosi cha wachezaji wa akiba wa Randers
kitakachocheza na AC Horsens Jumanne ijayo kwenye Ligi ya Wachezaji wa
Akiba ndani ya Ligi Kuu ya Taifa hilo 'Danish Superliga'.
Comments
Post a Comment