Mwili wa binadamu unaweza kupatwa na sumu au takataka zisizohitajika na
kwa namna mbili; kupitia mazingira tunayoishi kama vile viwanda, migodi
na maeneo mengine hatarishi ama kupitia vyakula na vinywaji ambavyo
tunatumia kila siku.
Sumu au takamwili,zinaweza kuingia mwilini kupitia dawa mbalimbali hasa
za kizungu tunazotumia kujitibu magonjwa mbalimbali. Mwili huzalisha
sumu au takamwili (free radicals) kila mara kunapofanyika mmeng’enyo wa
chakula mwilini mwako.
Hizi ni ishara zinazoweza kuashiria mwili wako umeingiwa na takamwili:
-Uchovu sugu
-Maumivu ya maungio
-Msongamano puani
-Kuumwa kichwa kila mara
-Tumbo kujaa gesi
-Kufunga choo au kupata choo kigumu
-Kukosa utulivu
-Matatizo mbalimbali ya ngozi ikiwemo chunusi
-Pumzi mbaya
-Mzunguko wa hedhi usio sawa
-Kuishiwa nguvu
-Kushindwa kupungua uzito
-Kupenda kula kula kila mara
Hizi ni njia 10 zinazoweza kuondoa sumu mbalimbali mwilini:
1. Fanya mlo wako mmoja wa siku kuwa ni matunda pekee
Amua moja ya mlo wako kwa siku uwe ni matunda pekee bila chakula kingine
zaidi. Unaweza kuamua ama chakula cha asubuhi au cha jioni kuwa ni
matunda pekee,Pia utumie maji ama juisi kama kinywaji chako.
2. Kula vyakula vya asili zaidi kuliko vya viwandani
Ili kuepuka sumu au takataka nyingine kirahisi kuingia katika mwili,
basi pendelea kula vyakula vya asili vinavyopikwa nyumbani na sio vya
kwenye makopo ama madukani.
3. Fanya masaji
Wengi tunaichukulia masaji kama kitu cha starehe tu (relaxation) lakini
unaweza kutumia masaji kama njia mojawapo ya kuondoa sumu mwilini na
utafanikiwa kwa muda mfupi sana.
4. Kunywa maji mengi kila siku
Sababu kubwa ya watu wengi kutengeneza sumu au taka mwilini mwao ni
kutokunywa maji mengi kila siku. Maji ni kiungo muhimu katika maisha
yetu na inashauriwa utumie zaidi ya lita 3 kwa siku.Kumbuka asilimia 94
ya damu yako ni maji, asilimia 85 za ubongo wako ni maji, hivyo ili
kusafisha damu na mwili kwa ujumla ni lazima unywe maji ya kutosha kila
siku.
5. Epuka chai ya rangi na Kahawa
Epuka kunywa chai ya rangi ama kahawa na badala yake tumia chai yenye
tangawizi au mdalasini au mchaichai. Chai ya rangi na kahawa vina
kaffeina ambayo kwanza huyasukuma maji nje ya mwili kwa haraka na
kuuacha mwili bila kuwa na maji ya kutosha kwa ajili ya kazi zake.
6. Fanya mazoezi ya viungo
Mazoezi ya viungo ni jambo la muhimu na laulazima kama ilivyo chakula.
Iwe unaumwa au huumwi, iwe una uzito kuzidi au una uzito wa kawaida
hakikisha unapata muda wa kufanya mazoezi.Hakikisha jasho linakutoka la
kutosha na iwe ni jambo la kila mara na siyo unaenda jumamosi na
jumapili (weekend) tu, hiyo haitoshi, fanya mazoezi mara 4 mpaka mara 5
kwa wiki.
7. Kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi
Vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi ni pamoja na parachichi, ndizi, peazi,
karoti, pilipili hoho, mchele wa brown (ule wanashauriwa watu wa
kisukari wautumie), maharage meusi, njegele, tende, viazi vitamu, tufaa
(apple), machungwa, ugali wa dona pia mkate wa unga wa ngano ambao
haujakobolewa.
8. Funga kula
Kupunguza sumu mwilini kwa haraka ni kufunga kula kabisa kutwa nzima.
Ukifunga kula mwili unalazimika kuvitumia vile vilivyomo ndani yake bila
kushughulika kuvisaga vingine vipya unavyokula. Unaweza kufunga kula
kabisa kwa wiki mara 2 hata 3 ili kuondoa au kupunguza sumu, hii inaweza
kuwa pia ni njia mojawapo ya kufanya maombi na kujiweka karibu na
muumba wako.
9. Pata usingizi wa kutosha kila siku
Moja ya vitu vinaweza kukupelekea kuwa na sumu mwilini au takataka
nyingi ni pamoja na kutokulala muda wa kutosha kila siku. Usingizi
haukopwi na huwezi kuwa na ufanisi katika kazi zako kama hupati usingizi
wa kutosha kila siku.Unapopata muda wa kutosha wa kulala masaa 7 mpaka 8
kwa siku unaupa mwili wako nafasi ya kutosha ya kupumzika na kujiripea
upya na hivyo ndivyo sumu na takataka nyingine zinavyoweza kukutoka
kirahisi.
10. Epuka mazingira hatarishi kwa sumu
Kuna mazingira yanajulikana wazi kuwa ni vyanzo vya sumu mwilini. Maeneo
ya migodi ya madini, maeneo yenye viwanda vingi, maduka yanayouza dawa
za kilimo nk.Maeneo haya yanafaa kukaa mbali na makazi ya binadamu kwa
usalama wa afya zetu.
Chanzo: Dr.Fadhil paulo
Comments
Post a Comment